SERIKALI imetuma kikosi maalum cha wapelelezi mjini Siakago, Kaunti ya Embu, kufuatia wingu la visa vya ghasia ambavyo vimesababisha mali yenye thamani ya mamilioni kuharibiwa na wakazi kadhaa kujeruhiwa.
Machafuko yalizuka wakati wafanyabiashara wa Meru na Embu walipokabiliana vikali mjini humo, Mbeere Kaskazini, kuhusu uhasama wa kibashara.
Kwenye ghasia hizo, majengo ya kibiashara, magari na mali nyingineyo iliteketezwa.
Taharuki ilitanda huku makundi hayo mawili hasimu yakipigana na kusitisha biashara kwa siku mbili katika mji ambao kwa kawaida huwa wenye shughuli nyingi.
Waziri wa Huduma za Umma, Geoffrey Ruku, alitangaza kuwa makachero wanatazamiwa kuendesha uchunguzi wa kina kubaini ukweli kuhusu tukio hilo.