MADEE: "Watu Wanadai Tunajipendekeza Kwa Rais na CCM"

Msanii wa Bongo Fleva, Madee, amewaomba watanzania hususani mashabiki wao kutambua kuwa wao kama wasanii pia wana haki ya msingi kuonesha mapenzi yao na kujihusisha na shughuli za chama cha kisiasa wanachokipenda.

Hayo yamezungumzwa na msanii huyo katika usiku wa Hafla ya Harambee kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam, Jumanne ya Agosti 12, ambapo wasanii mbali mbali na wadau wengine walihudhuria kwa ajili ya kukiunga mkono chama hicho.

Madee ameongeza kuwa, yeye na baadhi ya wasanii mbali mbali wamekuwa wakijitoa kwa ajili ya CCM ikiwa ni kupongeza na kushukuru juhudi mbali mbali ambazo zinafanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama, hasa katika kuwainua wasanii mbali mbali na kuthamini uwepo wao katika Sekta ya Uchumi

Kushiriki kwao kumekuwa kukibezwa na baadhi ya mashabiki wao na wananchi wengine kwa madai kuwa wamekuwa wakijipendekeza kwa Rais pamoja na CCM kiujumla, kitu ambacho wanakipinga vikali

“Samia Kings inajumuisha wasanii wa aina tofauti. Kuna waigizaji, wapiga picha, waimbaji n.k ambao sote tunajumuika katika project hii ya sasa kuhakikisha tunaunga mkono Juhudi za Mheshimiwa Raisi katika kujitoa kwake kwa wasanii mbali mbali japo watu wanabeza kwamba tunajipendekeza kwa Rais, tunajipendekeza kwa CCM, kitu ambacho sio kweli” Alisema Madee

 


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii