Upande wa Jamhuri kuomba kesi ya Lissu isirushwe live

Upande wa Jamhuri umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuzuia urushaji wa moja kwa moja wa mwenendo wa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, kwa lengo la kulinda utambulisho wa mashahidi.

Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, ametoa ombi hilo Jumatano mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga, akibainisha kuwa Mahakama Kuu tayari ilishatoa maagizo ya kuhakikisha mashahidi ambao ni raia wanalindwa dhidi ya utambulisho usioidhinishwa.

Kwa mujibu wa Katuga, maagizo ya Mahakama Kuu yalipiga marufuku uchapishaji au uwasilishwaji wa ushahidi wowote unaoweza kufichua utambulisho wa mashahidi raia wa kawaida bila ruhusa maalum ya mahakama hiyo.

“Ombi letu, pamoja na nia njema ya mahakama kuonesha mwenendo wa shauri kwenye vyombo vya habari, ni kwamba yafuatwe maagizo ya Mahakama Kuu. Ikiwa mshtakiwa atasomewa mashtaka, basi iwe kwenye mahakama ya wazi lakini bila matangazo ya moja kwa moja,” amesema Katuga.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii