Kesi ya Uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu inatarajiwa kusikilizwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Kesi hiyo ya uhaini ipo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franko Kiswaga ambaye alipanga leo Agosti 13 mwaka huu kutoa uamuzi juu ya hoja za Lissu na Jamhuri kuhusu kufutwa kwa kesi hiyo pamoja na baadhi ya mashahidi wa Jamhuri kuwa wa kificho/siri.
Mbali na hilo pia Upande wa Jamhuri unatarajiwa kuwasilisha taarifa yao leo juu ya uamuzi wa Mahakama Kuu ambayo ilikubaliana na maombi yao ya mashahidi (raia) kutoa ushahidi wao kwa siri.
Pia itakumbukwa wakati kesi hiyo ikitarajiwa kuunguruma Agosti 12 mwaka huu Mahakama Kuu ilitupilia mbali shauri la maombi ya Lissu ya kutaka kuwaona mashahidi katika kesi hiyo.
Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini akidaiwa kutenda kosa hilo April 3 mwaka huu kwa madai ya kuhamasisha kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.