Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Samandito Gombo, akiambatana na Mgombea wake mwenza Husna Abdallah, leo Agosti 13 mwaka huu amechukua fomu ya kuteuliwa kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Akizungumza na wanahabari mara baada ya kuchukua fomu hizo, Gombo amesisitiza kuwa vipaumbele vyake ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki bila ubaguzi, kwa wenye nacho na wasio nacho.
"Tanzania haki zimegawanyika, zimekuwepo haki za wenye nacho na haki za wasionacho. Sasa haki za wenye nacho ndo wale ambao unakuta keki ya Taifa wanakaa nayo vizuri na wasiokuwa nacho ndo wale ambao unakuta wanahangaika," amesema Gombo.
Ameongeza kuwa katika eneo hilo la haki, wananchi wamekuwa wakishindwa kuzipata katika huduma mbalimbali za kijamii.