Ukraine inastahili kuamua yenyewe kuhusu mstakabali wake

Viongozi kutoka katika mataifa ya Umoja wa Ulaya wamesisitizia haki ya raia wa Ukraine kuamua wenyewe kuhusiana na masuala ya mustakabali wa taifa leo.

Wito wa viongozi hao unakuja wakati huu zikiwa zimesalia siku tatu peke kabla ya Rais wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa Urusi Vladmir Putin kukutana.

"Sisi kama viongozi wa Umoja wa Ulaya, tunakaribisha juhudi za Rais wa Marekani kusaidia kumaliza uvamizi wa uchokozi wa Urusi nchini Ukraine pamoja na kupatikana kwa amani ya kudumu na usalama kwa kwa raia wa Ukraine," imesema taarifa ya EU.

Aidha wamesisitiza umuhimu wa kuheshimwa kwa sheria za kimataifa kuhusu uhuru wa ardhi ya nchi nyengine, wakipinga jaribio lolote la kuchukua ardhi ya taifa lengine kwa nguvu.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na viongozi wa EU wanatarajiwa Jumatano ya wiki hii kukutana na Rais Donald Trump.

Trump hajaweka wazi agenda ya mkutano wa wiki hii na Putin katika jimbo la Alaska, akisema analenga kuutumia mkutano huo kupima fikira za Putin kuhusu kumaliza mapigano nchini Ukraine.

Zelensky kwa upande wake akataa mapendekezo ya kuachia ardhi ya Ukraine kwa Urusi, Trump kwa upande wake akisisitiza ni lazima hilo lifanyike.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii