Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata Shehena kubwa ya dawa mpya ya Kulevya aina ya Mitragyna speciosa, yenye Mifuko 756 yenye uzito wa jumla wa kilogramu 18,485.6, sawa na takriban tani 18.5 Shehena hiyo ilipatikana ikiingizwa nchini kama Mbolea.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, ametoa taarifa hii leo August 13, kwamba Watuhumiwa Saba wamekamatwa, wakiwemo raia Wawili wa Sri Lanka, Jagath Prasanna Madduma Wellalage (46) na Santhush Ruminda Hewage (25), Watanzania waliokamatwa ni Riziki Abdallah Shawej (40), Andrew Athanas Nyembe (34), Mariam Shaban Mgatila (40), Ramadhan Sanze Said (57), na Godwin Melchory Maffikiri (40).
“Dawa hizi zilikamatwa kwenye Kontena lenye ukubwa wa futi 40 zikitoka Sri Lanka, hii ni mara ya pili kukamatwa kwa aina hii ya dawa mpya za kulevya, Mwezi Juni mwaka huu, tulikamata mifuko 450 yenye uzito wa tani 11.5 kutoka Sri Lanka,” amesema Lyimo na kuongeza kuwa “jumla ya dawa zilizokamatwa kwa kipindi kifupi ni kilogramu 30,082.03, sawa na takriban tani 30.
Lyimo alieleza kuwa Mitragyna speciosa ni dawa mpya ya kulevya inayotokana na mmea unaojulikana kama Kratom, unaopatikana zaidi katika nchi za Kusini Mashariki mwa Asia, Dawa hii ina madhara sawa na dawa za jamii ya Afyuni kama Heroin na Morphine, ikihusisha kuathiri mfumo wa fahamu, uraibu, na hata vifo vya ghafla.
Kamishna Jenerali alisisitiza kuwa DCEA itaendelea kufuatilia kwa karibu dawa hii na kuelimisha umma kuhusu madhara yake, huku ikishirikiana na vyombo vya usalama kuhakikisha watuhumiwa wanashughulikiwa kisheria.