China imeanza rasmi maonesho Michezo ya Roboti

China imeanza maonesho ya Michezo ya siku tatu kwa Roboti wenye umbo la binadamu, ikilenga kuonesha maendeleo katika teknolojia ya akili bandia na uhandisi wa roboti, Mashindano haya ya World Humanoid Robot Games inazileta pamoja timu 280 kutoka nchi 16, zikiwemo Marekani, Ujerumani na Brazil.

Roboti hao wanashindana katika Michezo kama Kandanda, Riadha, na Tenisi ya Meza, sambamba na changamoto maalumu za kiufundi kama kupanga dawa, kushughulikia mizigo na kufanya usafi, ambapo kati ya timu hizo 192 zinawakilisha Vyuo Vikuu na 88 zinatoka katika Makampuni binafsi, yakiwemo Makampuni ya Kichina kama Unitree na Fourier.

Serikali ya Manispaa ya Beijing ni miongoni mwa Waandaaji, ishara ya kipaumbele kinachowekwa na China katika sekta ya roboti na azma yake pana katika maendeleo ya akili bandia na mfumo wa otomatiki.

Msukumo huu wa teknolojia pia unakuja wakati taifa hilo likikabiliwa na changamoto ya kuzeeka kwa idadi ya watu na kasi ndogo ya ukuaji wa uchumi.

Kwa mwaka uliopita pekee, Serikali ya China imetoa ruzuku inayozidi dola bilioni 20 kwa sekta ya roboti na ina mpango wa kuanzisha mfuko wa Yuan Trilioni moja (takribani dola bilioni 137) kusaidia kampuni changa za AI na roboti.

Katika miezi ya hivi karibuni, China imeandaa matukio kadhaa makubwa ya roboti, yakiwemo yale inayodai kuwa ni mbio za kwanza duniani kwa roboti wenye umbo la binadamu, mkutano wa roboti na kufunguliwa kwa maduka ya rejareja maalum kwa roboti hao. 

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii