Sakata la ndugu wa marehemu, Mohamed Ally (20), mkazi wa Jiji la Arusha, mwili wake kudaiwa kuzuiwa kuchukuliwa na ndugu zake katika Hospitali ya Rufani ya Mount Meru, limechukua sura mpya.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo ya Mkoa wa Arusha, Dk. Kipapi Milambo, akizungumzia sakata hilo juzi alisema menejimenti haikuzuia mwili huo, kwa kuwa familia iliruhusiwa kuuchukua asubuhi ya Agosti 11 mwaka huu.
Alisema familia walilipa bili (malipo yote) yanayotokana na gharama za tiba na kukabidhiwa mwili bila tatizo lolote.
Kwa mujibu wa Dk. Milambo, Mohamed alifariki dunia kutokana na ajali ya barabarani, alifikishwa hospitalini hapo usiku wa Agosti 9, 2025, saa 4:15 usiku na kuanza kupatiwa matibabu ya dharura.
“Hizo taarifa zilizosambaa mitandaoni, zikidai kwamba Mount Meru ilizuia mwili wa kijana aliyefariki dunia kutokana na ajali kwa sababu ya kutokulipwa bili ya matibabu, sio za kweli.
…Hali ya afya ya kijana huyo ilizidi kuwa mbaya na alifariki dunia saa 8:00 usiku wa siku hiyo hiyo, ambapo ndugu walifika kuchukua mwili asubuhi ya Agosti 11 mwaka huu, na walilipa bili hiyo na kukabidhiwa mwili bila tatizo lolote.”
Dk. Milambo, alisema gharama alizolipa zilihusisha matibabu ya vipimo vya X-ray, CT scan na maabara, ambapo gharama za huduma hizo zilifikia Sh. 910,000.
“Wakati wa kuchukua mwili, baadhi ya vijana wa bodaboda waliokuwa na ndugu wa marehemu walifanya vurugu katika eneo la mochwari, wakipinga bili waliyopewa, lakini hakuna ucheleweshaji wa makusudi uliofanyika,”alisema.
Kutokana na sakata hilo, menejimenti ya Hospitali ya Mount Meru, imesisitiza kuwa inafuata maagizo ya serikali ya kutokuzuia miili ya marehemu, kwa sababu ya madeni, na itaendelea kutoa huduma bila kikwazo cha fedha.
Juzi, makundi ya vijana walikwenda hospitalini hapo kuwasindikiza ndugu na jamaa kuuchukua mwili huo, walipinga gharama hizo na kususia kuuchukua mwili wa Mohamed.