Sugu yataka Lissu aachiwe bila masharti yoyote

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi (Sugu), ametaka Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Tundu Lissu aachiwe bila masharti yoyote kwani yeye sio Muhaini.

Akiongea na kwa njia ya mtandao leo, Sugu amesema kesi hiyo inamaliza pesa bure pamoja na kuendelea kuleta taharuki kwenye Taifa na kuifanya Tanzania kuandikwa kwenye Vyombo vya Habari vya Kimataifa na kuiwekea doa taswira ya Tanzania duniani.

Kwa upande mwingine, Sugu amesema Wananchi wana haki ya kuchagua Viongozi wao kidemokrasia na sio kuwekewa Viongozi wasiowataka na kusisitiza kuwa kitendo cha Wananchi wengi kutokujitokeza kupiga kura katika chaguzi zilizopita ni ishara ya kupinga mfumo wa Kisiasa usiozingatia mageuzi ya kweli.

Mbunge huyu wa zamani wa Mbeya Mjini ametoa wito kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kulitilia maanani jambo hili na kufanya mabadiliko ya sheria za Uchaguzi kabla ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025 na kusisitiza kuwa sasa ni wakati wa kufanya uchaguzi wa haki na ulionyooka kwa kuwapa nafasi Wananchi kuwachagua Viongozi wanaowataka ili kuendelea kudumisha Amani, Utulivu na kulijenga Taifa kwa ushirikiano wa Watanzania wote.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii