SERIKALI chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imepeleka Mkoani Lindi Mradi wa Umeme Jua wenye thamani ya Sh milioni 801.74 katika visiwa vyote vitano vilivyopo wilayani Kilwa ikilenga kuongeza upatikanaji wa umeme katika maeneo hayo ambayo yapo mbali na Gridi ya Taifa na kuhamasisha matumizi ya teknolojia safi kupitia mifumo ya umeme jua.
Akizungumza wakati akipokea taarifa ya mradi huo Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Zuwena Jiri amekiri kupokea mradi huo na kutoa wito kwa wananchi mkoani humo hasa wakazi wa Visiwani kuchangamkia fursa hiyo kwani tayari Serikali imetoa ruzuku.
“Kila kaya itakuwa na mfumo wake wa kujitegemea, wito wangu kwa wananchi hasa wakazi wa visiwani tuchangamkie fursa iliyokuja, kama mmoja angekuwa anafunga mwenyewe mfumo wa umeme jua inawezekana ikawa gharama kubwa sana lakini Serikali imetoa ruzuku mpaka asilimia (75%),” amesema Zuwena.
Sambamba na hilo Zuwena amewataka wananchi wa Mkoa wa Lindi kuchangamkia fursa ya Majiko Banifu ambapo serikali imetoa ruzuku ya asilimia 85 na kufanya gharama ya Jiko moja kuuzwa kwa Sh 9000 tofauti na bei halisia Sh 60000.
Kwa upande wake, Meneja wa Teknolojia za Nishati kutoka REA, Mha. Michael Kyessi amesema mradi unategemea kusambaza Majiko Banifu 5,576 kwa Mkoa wa Lindi ambapo majiko 1,115 yatagawanywa kwa kila wilaya.
“Gharama ya mradi kwa mkoa wa Lindi ni Sh 346,560,000.00 ambapo serikali itatoa ruzuku ya shilingi 294,576,000.00 . Mtoa huduma ni Tango Energy Ltd ambapo jumla ya majiko banifu 5,776 yatauzwa kwa wananchi kwa bei ya ruzuku. Gharama ya jiko moja ni Sh 60,000 kabla ya ruzuku, hivyo serikali itatoa ruzuku ya asilimia 85 sawa na Sh 51,000 na mwananchi atanunua jiko hilo kwa shilingi 9,000. Majiko haya yatasambazwa katika wilaya tano za Mkoa wa Lindi,” amesema Mha. Kyessi.
Kuhusu mradi wa jua ambao utafikia kaya 1,227 ndani ya visiwa vitano mkoani humo, Mha. Kyessi amebainisha mifumo hiyo imegawanyika katika mafungu matatu ya uwezo wa nishati ambayo ni 50Wp, 80Wp na 100Wp. Jumla ya mifumo ya 50Wp ni 736, 80Wp ni 307 na 100Wp ni 184.