JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watu tisa kwa tuhuma za utapeli na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kupitia mitandao ya kijamii ya Facebook na WhatsApp.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga alisema watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti Agosti 18, katika mitaa ya Nsalala na Mapelele iliyopo Kata ya Nsalala, mji mdogo wa Mbalizi.
Watuhumiwa wanne kati ya hao walikuwa wanawadanganya watu kupitia mitandao hiyo kuwa wanatafuta wafanyakazi wa kuuza duka la jumla liitwalo Kajala lililopo Dar es Salaam.
Aidha, watuhumiwa wengine watatu walikuwa wakitumia simu zao kuomba fedha kwa watu wakidai wao ni wafanyabiashara wa kuuza bidhaa mbalimbali kwa bei rahisi maarufu “Tuma kwenye Namba hii”.
Vilevile watuhumiwa wawili wafanyabiashara walikamatwa wakijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwa kuwarubuni na kuwachangisha fedha watu mbalimbali ili wajiunge na kuwa wamiliki wenza wa kampuni ijulikanayo Q NET ya nchini Malaysia.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni pamoja Nemia Njonga (23) fundi rangi, mkazi wa Mwakapangala, Ombeni Ambilikile (22) dereva bodaboda, mkazi wa Nsalala, Jacob Peter (23) fundi rangi mkazi wa mwakapangala na Baraka Mgala (22) dereva bodaboda na mkazi wa mtaa wa Mbalizi.
Wengine ni mkazi wa Mbalizi, Lusajo Jeremiah (45), Adili Mbeyale (19) mkazi wa Mbalizi pamoja na Shaban Yasin (23) mkazi wa mtaa wa mshikamano, Ester Kimaro (28) mfanyabiashara na mkazi wa Nzovwe pamoja na Abdi Awadhi (21).