Mteja aliyeihujumu Tanesco akamatwa Geita

Katika zoezi la ukaguzi wa mita lililofanyika katika Kata ya Nkome Wilaya ya Geita Mkoani humo, wakaguzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wamebaini udanganyifu wa matumizi ya umeme kutoka kwa mteja mmoja aliyekuwa anatumia mita ya njia tatu (three phase). 

Kwa mujibu wa msimamizi wa kitengo cha ukaguzi wa mita (TANESCO) Juma Mbuto, amesema mteja huyo Joseph Bukerebe alichepusha umeme kwa kuunganisha moja kwa moja waya kutoka kwenye chanzo cha umeme cha TANESCO kwenda kwenye kiwanda chake cha kuzalisha barafu, bila kupitia kwenye mita ya kupima matumizi, hali ambayo imesababisha njia mbili kati ya tatu kutosoma kiwango halisi cha matumizi ya umeme.

Baada ya kubaini udanganyifu huo TANESCO imesitisha huduma ya umeme kwa mteja huyo huku taratibu za kisheria zikiandaliwa ili kumfikisha mahakamani kwa makosa ya wizi wa umeme uliosababisha hasara kwa shirika.

Mbali na kushitakiwa mteja huyo pia atawajibika kulipia gharama zote za umeme aliotumia kinyume cha utaratibu pamoja na faini zitakazowekwa kwa mujibu wa sheria.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii