Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti amesema mashamba ya uzalishaji mifugo ya Serikali lazima yaachwe yafanye shughuli za kiserikali kwa ajili ya manufaa ya taifa zima huku akiwaonya wananchi wanaoshirikiana na wavamizi katika mashamba ya ufugaji Misungwi mkoani Mwanza.
Mnyeti amesema hayo leo Jumanne Julai 8, 2025 alipofanya ziara katika shamba la uzalishaji mifugo la Serikali Mabuki lililopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, ambapo amesema mifugo iliyopo katika mashamba ya hayo ni kama mbegu ambazo lazima kuzitunza ili kutoharibu mbegu za asili za mifugo.
“Mashamba ya serikali ni rasilimali za Watanzania wote lazima kulinda kwa pamoja, hizi ng’ombe ni kama mbegu tukiziharibu hizi mbegu ni kwamba tunaharibu kabisa ng’ombe zetu za asili.”
Hii ni baada ya taarifa ya kuwepo kwa uvamizi wa mifugo kuingizwa katika shamba la uzalishaji mifugo la Serika Mabuki kwa ajili ya malisho.
“Ng’ombe 20,000 waliovamia shamba la Mabuki siyo wa wafugaji wa Misungwi isipokuwa wafugaji wa Misungwi wamekuwa siyo waaminifu kwa kuyaficha makundi ya ng’ombe kutoka nje ya Misungwi halafu wanajifanya ni ng’ombe wao,” amesema Mnyeti.
Ameongeza kuwa hayupo tayari kuwatetea wafugaji wanaoingiza mifugo kwenye mashamba ya uzalishaji mifugo ya serikali kwa kuwa hata yeye ni mfugaji lakini anaheshimu maeneo yaliyotengwa na serikali, yakiwemo mashamba ya uzalishaji mifugo ya serikali na kwamba hayuko tayari kupeleka mifugo yake kwenye mashamba hayo bila kufuata utaratibu wa serikali.