FAMILIA ya Brian Kimutai, mwandamanaji mwenye umri wa miaka 21, aliyedaiwa kupigwa risasi na afisa wa polisi wakati wa maandamano ya Saba Saba huko Kitengela, ilikwama na mwili wake ndani ya gari katika mochari ya Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Kitengela kwa saa kadhaa baada ya usimamizi wa hospitali hiyo kukataa kuupokea mwili huo.
Brian, ambaye alikuwa mwendesha bodaboda, alitangazwa kufa alipofikishwa katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Kitengela, ambako alikimbizwa wakati wa maandamano ya Jumatatu yaliyotikisa mji huo.
Baadaye, waandamanaji waliokuwa na hasira walizingira hospitali hiyo kwa takriban saa tano wakijaribu kuwazuia maafisa wa polisi kuufikia mwili huo.
Jioni, familia ikisaidiwa na waandamanaji walibeba mwili kwa gari la binafsi hadi nyumbani kwao, umbali wa mita chache kutoka hospitali hiyo.
Jumatatu asubuhi, familia ilirudisha mwili huo katika mochari ya hospitali hiyo
Lakini taarifa zinasema usimamizi wa hospitali ulikataa kuupokea mwili huo, hali iliyosababisha mvutano.
Mwili huo, uliokuwa umefungwa kwa mashuka, ulikuwa katika kiti cha abiria cha gari aina ya station wagon.
Bi Ann Nyawira Gikunju, mama ya Brian, aliambia gazeti la Taifa Leo kuwa aliamua kupeleka mwili wa mwanawe nyumbani baada ya kupata habari kuwa maafisa wa DCI walikuwa na mpango wa kuuhamisha hadi mochari ya jiji bila ruhusa yake.
“Tulikesha na mwili ukiwa ndani ya gari usiku kucha kwenye egesho la nyumba ya kupanga. Hatukuwaruhusu polisi waupeleke mochari ya mbali,” alisema Bi Gikunju.
“Maafisa wa polisi wananisumbua baada ya kumuua mwanangu. Nitapigania haki yake hadi mwisho,” aliongeza.
Mama huyo alisema mwanawe alikuwa mhanga wa uhasama wa kibinafsi kati yake na afisa wa polisi aliyempiga risasi, akidai kwamba alikuwa ametishiwa na afisa huyo aliyefahamika.
Baada ya mvutano wa takriban saa mbili, maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) walipoukagua mwili huo, ulihamishiwa mochari ya Hospitali ya Shalom, Athi River, Kaunti ya Machakos.