REA kuhakikisha 80% wanatumia nishati safi ifikapo 2034

MKURUGENZI Mkuu na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Hassan Saidy amesema wakala huo umejizatiti kuhakikisha 80% ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Amebainisha hayo Julai 07 mwaka huu  katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) Jijini Dar es Salaam ndani ya banda la Maonesho la Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

“REA inalo jukumu la kuhakikisha maeneo yote ya vijijini yanapata aina zote za nishati safi zinazotumika nchini ikiwemo; umeme, nishati safi ya kupikia pamoja na bidhaa za mafuta ya petroli na dizeli na hili linafanyika kupitia miradi mbalimbali ambayo baadhi imekamilika na mingine ipo katika hatua tofauti tofauti za utekelezaji,”alibainisha Saidy.

Alisema mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia umeelekeza ifikapo mwaka 2034; angalau 80% ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia na REA ni miongoni mwa taasisi zilizopewa jukumu la kuhakikisha lengo hilo linafikiwa.

Hassan Saidy aliongeza kuwa kwa sasa takriban asilimia 96 ya wananchi maeneo ya vijijini wanatumia kuni na mkaa kupikia na kwamba jukumu lililopo ni kuhakikisha wananchi hao wanaachana na matumizi ya nishati zisizo salama na kuanza kutumia nishati safi na salama.

Alitaja hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na REA ikiwemo uhamasishaji na uelimishaji wananchi kufahamu athari za kutumia nishati isio salama pamoja na kuwafahamisha faida za kutumia nishati safi ya kupikia, kuwarahisishia wananchi upatikanaji wa bidhaa za nishati safi jirani na maeneo yao na kuwezesha teknolojia za nishati yenyewe.

“Kuna dhana imejengeka kwamba nishati safi ya kupikia ni gharama kuliko nishati zingine dhana ambayo haina ukweli kwa 100% kwani kwa sasa kuna teknolojia zilizoboreshwa ambazo zinazuia upotevu wa nishati wakati wa kupika hivyo kuwapunguzia gharama watumiaji,” alifafanua Saidy.

Aliongeza kuwa watu wengi hawaangalii gharama nyingine kama muda wanaotumia kusaka kuni na madhila mengine wanayokutana nayo huko porini wakati wakisaka kuni.

Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha REA kutekeleza jukumu la kusimamia upatikanaji wa nishati safi ya kupikia hasa ikizingitiwa kuwa yeye ni kinara wa nishati safi ya kupikia.

Katika hatua nyingine alibainisha baadhi ya mafanikio ambayo yamepatikana tangu kuanza kutekeleza mkakati huo wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambayo ni pamoja na kuwezesha wananchi maeneo mbalimbali vijijini kuhama kupitia ruzuku iliyotolewa ya asilimia 50 kwenye majiko ya gesi ya kilo 6 na vichomeo vyake.

“Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia ilitoa ruzuku ya 50% kwenye mitungi ya gesi ya kupikia ipatayo 452,000 ambayo imeshaanza kusambazwa kwenye mikoa yote Tanzania Bara na zoezi linaendelea; sambamba na mitungi 110,000 ambayo ilisambazwa mwaka juzi kupitia Wabunge kwenye majimbo yao,” alisema Mhandisi Saidy.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii