SERIKALI imetangaza kuwa maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yamefikia ukingoni, baada ya kupitia mchakato wa hatua mbalimbali kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema hayo Dar es Salaam Julai 8, 2025 wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu hatua zilizopitiwa hadi kufikia maandalizi ya uzinduzi rasmi wa Dira hiyo.
Akieleza kwa kina kuhusu safari ya kuandaa dira hiyo, Prof Mkumbo amesema kuwa mchakato ulianza rasmi Februari hadi Machi 2023 kwa kuandaa miongozo ya uandishi, ambapo uzinduzi rasmi wa maandalizi hayo ulifanywa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, kwa niaba ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan mnamo Aprili 3, 2023. Kwahiyo hatua 12 kati ya 13 za maandalizi ya dira hiyo tayari zimekamilika.
Prof Mkumbo amezitaja hatua zilizokwishakamilika kuwa ni kuandaa na kuidhinisha miongozo ya uandishi wa Dira, ambayo ilikamilika kati ya Februari hadi Machi 2023, uzinduzi rasmi wa mchakato wa kuandika Dira uliofanywa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Aprili 3, 2023, kuunda vyombo vya kitaasisi kusimamia uandishi wa Dira (Sekretarieti, Timu Kuu ya Kitaalamu, na Kamati ya Uongozi chini ya Waziri Mkuu) na tathmini ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2025.
Hatua zilizofuata zilikuwa ni ushirikishwaji wa wananchi na wadau, ambapo zaidi ya watu milioni moja walifikiwa kukusanya maoni, ujifunza kutoka nchi mbalimbali duniani (kama Botswana, Vietnam, Mauritius n.k.), kuandikwa kwa rasimu ya kwanza ya Dira na wataalamu na uzinduzi wa Rasimu ya Kwanza uliofanywa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.
Baada ya Uzinduzi wa Rasimu ya kwanza ya Dira 2050, uchambuzi wa maoni juu ya Rasimu ya Kwanza ulifuata kwa ajili ya maridhiano ya kitaifa.
Amesema hatua zingine ilikuwa ni kuandaliwa kwa Rasimu ya Pili ambayo ilikabidhiwa rasmi kwa Waziri Mkuu, Idhini ya Baraza la Mawaziri iliyotolewa tarehe 22 Juni 2025 na kuwasilishwa kwa Dira Bungeni, ambapo Bunge liliridhia rasmi, ikiwa ni hatua ya kuiwekea ulinzi wa kikatiba kwa ajili ya utekelezaji wa muda mrefu.
“Rais alisisitiza Dira hii ipelekwe Bungeni ili iwe na uhalali wa kitaifa na kulindwa na mihimili ya dola. Hii ni kwa sababu itatekelezwa na marais wasiopungua wawili, watatu au wanne,” amefafanua Pro Mkumbo.
Waziri Mkumbo ameeleza kuwa sasa Serikali inajiandaa kwa uzinduzi rasmi wa Dira hiyo, hatua ya mwisho katika mchakato huo.
Uzinduzi utafanyika mjini Dodoma tarehe 17 Julai 2025 na utaongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, ambaye ndiye aliyetilia mkazo umuhimu wa kuwa na dira itakayojenga msingi wa Tanzania ya viwanda, TEHAMA, na maendeleo jumuishi ifikapo mwaka 2050.