Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 kuzinduliwa julai 17

 RAIS Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 Julai 17, 2025, akiweka rekodi ya kuwa Rais wa Pili Tanzania kusimamia na kuratibu uandikaji wa dira hiyo ya miaka 25 ijayo.

Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Mjini Dodoma.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, leo Julai08, 2025 Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, ameeleza kuwa uzinduzi wa Dira 2050 unafuatia hatua muhimu ya Baraza la Mawaziri kuidhinisha dira hiyo pamoja na kuridhiwa kwa Dira 2050 na Bunge la Tanzania.

“Kwa mara ya pili nchi yetu inaandaa Dira ya Maendeleo ambayo haina mwelekeo wa kiitikadi ya chama cha siasa na Rais Samia Suluhu Hassan anakuwa Rais wa Pili kuandika Dira, Rais wa Kwanza alikuwa Hayati Benjamini Mkapa,” amesema Prof Mkumbo.

Aidha, Prof Kitila amebainisha kuwa wakati wa uzinduzi wa Dira 2050, Watanzania ndipo watakapopata fursa pia ya kufahamu yaliyomo ndani ya Dira hiyo, akiwashukuru wadau mbalimbali kwa ushiriki wao kikamilifu katika hatua zote 12 za Mchakato wa uandaaji wa Dira hiyo ya Maendeleo ya Taifa.

Katika hatua nyingine, Prof Mkumbo ameeleza kuwa Rais Samia alielekeza dira hiyo kupitishwa bungeni, ikiwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo ili kuweka kinga ya kisheria kwa Dira 2050 katika kudhibiti Serikali zijazo kukiuka ama kuachana na yaliyomo katika Dira hiyo kwa miaka 25 Ijayo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii