Hatua ya Elon Musk kuzindua chama kipya cha siasa chazua moto kwa Donald Trump

Utajiri wa Mkurugenzi Mtendaji wa Tesla na SpaceX, Elon Musk, umepungua kwa kiasi cha dola bilioni 15 kwa siku ya leo pekee baada ya hisa za kampuni ya Tesla kuporomoka kwa karibu asilimia 7 na kushuka kwa takriban dola 21.

Kulingana na Bloomberg Billionaires Index, imesema licha ya kupungua kwa kiwango hicho cha fedha Musk bado anaongoza kwa utajiri duniani.

Tukio hili linajiri baada ya Musk kuzindua chama chake kipya cha kisiasa hatua ambayo inaongeza moto kwenye mgogoro wake wa hadharani na Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye Musk alimuunga mkono kwa kiasi kisichopungua dola milioni 277 katika kampeni za uchaguzi wa urais wa mwaka 2024.

Hali ya hisa za Tesla imekuwa mbaya tangu kuapishwa kwa Trump Januari 2025, ambapo thamani ya kampuni hiyo imeshuka kwa asilimia 31, wakati S&P 500 ikiongezeka kwa karibu asilimia 4 katika kipindi hicho hicho.

Kwa mujibu wa taarifa za hivi karibuni, Tesla pia imekumbwa na kushuka kwa mfululizo kwa utoaji wa magari katika robo mbili za mwanzo wa mwaka 2025, hali ambayo haijawahi kushuhudiwa tangu mwaka 2022.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii