Chaguzi za UDA kupima nguvu zake Mlima Kenya

CHAGUZI za UDA zilizopangiwa kufanyika Mlima Kenya huenda zikawa jukwaa la wanasiasa kupimana ubabe hali ambayo inaweza kusababisha migawanyiko hata zaidi chamani kabla ya Uchaguzi Mkuu 2027.

UDA imeratibu chaguzi zake katika eneo la Mlima Kenya lenye idadi wengi ya wapigakura mnamo Januari 10, 2026. Chaguzi hizo za mashinani zinafanyika wakati ambapo Rais William Ruto amepoteza baadhi ya wandani wake wakuu eneo hilo.

Matokeo ya chaguzi hizo huenda yakatumika kupima umaarufu wa chama hicho katika eneo lililomwezesha Dkt Ruto kunyakua mamlaka kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Idadi ya watakaojitokeza na wanaogombea nyadhifa za uongozi wa chama hicho itakuwa muhimu kupima ushawishi wa UDA huku kukiwa na dhana kwamba eneo hilo limetema chama tawala.

Baadhi ya wandani wakuu wa Dkt Ruto eneo hilo wametangaza kumuunga mkono aliyekuwa naibu rais, Rigathi Gachagua, ambaye anapigia debe vikali chama chake cha DCP kama chama kipya cha eneo hilo.

UDA jana iliongeza muda wa usajili kwa wawaniaji wanaomezea mate nyadhifa mbalimbali za chama.

“Bodi inayosimamia Chaguzi Kitaifa ya UDA imetoa notisi rasmi kwa wadau wote, wanachama na wagombea kuhusu Kuongeza Muda Makataa ya Kujisajili kwa Awamu III ya Chaguzi za Chama.”

“Mnafahamishwa kwamba makataa ya kujisajili, yaliyopangiwa awali kukamilika Disemba 23, 2025, sasa yameongezwa muda hadi Disemba 31, saa sita kasoro dakika moja usiku. Muda huu wa ziada umeongezwa kuruhusu wanachama waliofuzu na wagombea wanaowania kukamilisha mchakato wa usajili,” alisema Mwenyekiti wa Bodi ya Uchaguzi wa UDA Anthony Mwaura kupitia taarifa.

Bw Mwaura alitaja sikukuu za Krismasi kuwa kiini cha kuongeza muda huo, lakini Taifa Leo ilibaini kwamba UDA haikuwa imevutia wagombea wa kutosha kufikia muda uliowekwa.

Chaguzi zilizopangwa kufanyika zitaendeshwa katika kaunti za Embu, Kiambu, Kirinyaga, Laikipia, Meru, Murang’a, Nyandarua, Nyeri na Tharaka Nithi.

Katika Bonde la Ufa, zitafanyika Baringo, Bomet, Elgeyo Marakwet, Kericho, Nakuru, Nandi, Trans Nzoia, Uasin Gishu na Samburu huku Magharibi zikifanyika Kakamega na Vihiga.

Baadhi ya viongozi wa UDA ambao yamkini wametengana na Dkt Ruto na huenda wanaelekea kutema chama hicho wanajumuisha Ndindi Nyoro (Kiharu), John Methu (Nyandarua), Joe Nyutu (Murang’a), Karungo Thang’wa (Kiambu), Benjamin Gathiru almaarufu Mejja Donk (Embakasi Kati), James Gakuya (Embakasi Kaskazini), James Murango (Kirinyaga), John Kinyua (Laikipia).

Baadhi ya viongozi wa UDA ambao kwa sasa wanamuunga mkono Bw Gachagua, kabla ya kufurushwa kwake Oktoba 2024, walikuwa wamedokeza mipango ya kugombea nyadhifa kuu.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii