UN yaichagua Tanzania kuandaa mafunzo ya kimataifa kwa maafisa wa jeshi

Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kimechaguliwa na Umoja wa Mataifa (UN) kuwa mwenyeji wa mafunzo ya kipekee kwa ajili ya maafisa wanadhimu wa jeshi kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa mafunzo hayo, Mkuu wa Chuo hicho, Brigedia Jenerali George Itang’are, alisema Tanzania inakuwa nchi ya pili duniani kuandaa mafunzo hayo, mara ya kwanza yakiwa yamefanyika nchini Italia.

"Kwa mara ya kwanza, Tanzania ni mwenyeji wa mafunzo haya ya maafisa wanadhimu wa jeshi yanayolenga kuwaandaa kuwa wakufunzi katika kozi mbalimbali za kijeshi. Pia, hii ni mara ya pili tu kwa mafunzo haya kufanyika tangu Umoja wa Mataifa ulipopitisha mtaala mpya wa mafunzo ya kijeshi," alisema Brigedia Itang’are.

Alibainisha kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa maafisa wenye uzoefu mkubwa, kwani yanalenga kuwaongezea uwezo wa kufundisha wanadhimu wengine katika nchi zao, kwa kutumia mbinu za kisasa zinazotambulika kimataifa.

Katika awamu hii ya mafunzo, jumla ya wanadhimu 22 kutoka Ghana, Nigeria, Botswana, Vietnam, Zambia na Tanzania wanashiriki, wakiwa wanafundishwa na wakufunzi kutoka Tanzania, Brazil, Bangladesh, Nigeria na Marekani.

Brigedia Itang’are alieleza kuwa mafunzo hayo yatafanyika kwa siku 10 kuanzia Julai 7 hadi 17, na yanafadhiliwa na Serikali ya Canada, ambayo pia imekuwa ikisaidia katika kuboresha uwezo wa chuo hicho.

Kwa upande wake, Mkuu wa Huduma Jumuishi za Mafunzo kutoka Umoja wa Mataifa, Harinder Sood, alieleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa kuongeza ufanisi katika operesheni za ulinzi wa amani duniani.

“Misheni za sasa za ulinzi wa amani zinakumbwa na changamoto nyingi. Hivyo, tunahitaji maafisa waliobobea na wenye ujuzi wa hali ya juu. Mafunzo haya yatawajengea uwezo wa kuwa wakufunzi katika nchi zao na hata kushiriki kutoa mafunzo katika mataifa mengine,” alisema Sood.

Alisema uteuzi wa Tanzania kuwa mwenyeji wa mafunzo hayo ni matokeo ya historia yake nzuri na ya kuigwa katika kushiriki kwenye operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa.

“Tanzania ni nchi yenye utulivu na mazingira rafiki kwa mafunzo ya kimataifa. Kwa miaka mingi imekuwa mshiriki muhimu katika juhudi za ulinzi wa amani, na tunatumaini itaendelea kuwa mshirika imara katika kuhakikisha dunia inakuwa na amani ya kudumu,” alisema.

Mafunzo haya yanatarajiwa kuongeza idadi ya wakufunzi mahiri wanaoweza kuandaa kozi za kijeshi ndani ya nchi zao na kuandaa vikosi vyenye ujuzi unaokidhi viwango vya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya operesheni za kulinda amani duniani.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii