Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb), ameshiriki hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Jamii ya Habari (WSIS+20) ulioanza tarehe 7 Julai 2025 katika Ukumbi wa Palexpo, uliopo mji wa Geneva nchini Uswisi.
Mkutano huo unalenga kutathmini mafanikio na changamoto za miaka 20 ya utekelezaji wa ajenda ya jamii ya habari duniani.
Mhe. Silaa ameongoza ujumbe wa Tanzania na amehudhuria mkutano huo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Katika mkutano huo, ujumbe wa Tanzania umepokea tuzo tatu za kimataifa kwa miradi ya TEHAMA inayotekelezwa nchini.
Tuzo ya kwanza imetolewa kwa mradi wa PharmAccess Zanzibar katika kipengele cha Afya Mtandao (e-Health) na kupokelewa na Waziri wa Afya kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui akishuhudiwa na Waziri Silaa.
Tuzo ya pili imekwenda kwa Mradi wa e-Mrejesho Platform wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) katika kipengele cha Serikali Mtandao (e-Government).
Tuzo ya tatu imetolewa kwa Mradi wa STEM 4 All kutoka Chuo Kikuu cha St. Joseph cha Tanzania, ulioshinda katika kipengele cha Sayansi Mtandao (e-Science).