Aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi wa Urusi Roman Starovoy, anashukiwa kujiua ikiwa ni saa chache baada ya Rais Vladmir Putin kumfukuza kazi, Vyombo vya habari vya Urusi vimeripoti.
Waziri huyo ameripotiwa kujiua saa chache tu baada ya kufutwa kazi na Rais Vladimir Putin kwa mujibu wa Shirika la habari la Serikali ya Nchi hiyo ambalo liliinukuu Kamati ya Taifa ya Uchunguzi.
Imeelezwa kuwa Roman Starovoy alijipiga risasi na kujiua leo Jumatatu akiwa ndani ya gari lake huko Odintsovo, Mji ulio magharibi mwa Moscow ambapo Kamati ya Uchunguzi imenukuliwa ikieleza maneno yafuatayo “mazingira ya tukio yanafahamika, dhana kuu ni kujiua.”
Japokuwa hakuna sababu rasmi iliyotolewa na Serikali kuhusu kufukuzwa kazi kwa Waziri huyo, wengi wamezungumzia mashambulizi yanayoendelea ya ndege za Ukraine dhidi ya Urusi yaliyosababisha machafuko na kukwamisha usafiri wa anga Nchini humo mwishoni mwa wiki iliyopita na kusababisha kufutwa kwa mamia ya safari za ndege na abiria waliokwama.
Starovoy aliteuliwa kuwa Waziri wa Uchukuzi wa Urusi mwaka 2024 ambapo kabla ya hapo alikuwa Gavana wa mkoa wa Kursk kwenye mpaka na Ukraine.