Rais Museveni, 80 aidhinishwa kuwania urais mwaka ujao

Chama tawala nchini Uganda NRM, mwishoni mwa juma kilimuidhinisha, Rais Yoweri Museveni, mwenye umri wa miaka 80 kuwa mgombea pekee wa kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Katika hotuba yake ya kukubali uteuzi wa chama, Museveni ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 40, amesema iwapo atachuguliwa tena, ataendeleza ajenda yake ya kuifanya Uganda kuwa bora zaidi.

Wapizani wa Museveni wanamtuhumu kwa kuiongoza Uganda kwa mkono wa chuma tangu mwaka wa 1986.

Tangu mwaka huo Museveni amekuwa akiibuka mshindi katika chaguzi zote, katiba ya nchi ikifanyiwa marekebisho mara mbili kuondoa mihula ya uongozi ilikumpa nafasi ya kuendelea kusalia madarakani.

Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine mpinzani wa Rais Museveni katika uchaguzi huo wa mwezi Januari, ameahidi kumshinda Museveni iwapo atapewa ridhaa na chama chake.

Wakati wa uchaguzi wa mwaka wa 2021, Wine, alipata asilimia 35 dhidi ya 59 ya Museveni.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii