Ufaulu kidato cha sita wafikia asilimia 99.95, ubora waongezeka

Ufaulu wa jumla wa wanafunzi wa kidato cha sita mwaka 2025 umeongezeka na kufikia asilimia 99.95, ambapo wanafunzi 125,779 kati ya 125,847 waliopata matokeo wamefaulu kwa kupata madaraja ya kwanza, pili, tatu na nne.

Akizungumza leo Julai 7, visiwani Zanzibar wakati wa kutangaza matokeo hayo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA)Profesa Said Mohamed, amesema ufaulu huo umeongezeka kwa asilimia 0.03 ikilinganishwa na mwaka 2024 ambapo wanafunzi 103,252 sawa na asilimia 99.92 walifaulu.

Ameeleza kuwa ubora wa ufaulu pia umeimarika, ambapo jumla ya watahiniwa 125,375 sawa na asilimia 99.62 wamepata madaraja ya kwanza hadi la tatu, ikiwa ni ishara ya mwelekeo chanya wa ubora wa elimu.

Profesa Mohamed amesema kati ya wanafunzi hao, waliopata daraja la kwanza ni 61,120 sawa na asilimia 48.57, huku 49,385 wakipata daraja la pili sawa na asilimia 39.24. Ongezeko la ubora wa ufaulu limefikia asilimia 0.22 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Amefafanua kuwa hakuna tofauti kati ya wanaume na wanawake katika ufaulu wa jumla, kwani wote wamefaulu kwa asilimia 99.95. Aidha, ubora wa ufaulu kwa wanawake ni asilimia 99.57 na kwa wanaume asilimia 99.68, tofauti ambayo ni ndogo sana.

Hata hivyo, Profesa Mohamed ameeleza kuwa wanafunzi 70 wamefutiwa matokeo yao kutokana na udanganyifu. Miongoni mwa sababu za kufutiwa matokeo ni pamoja na kuingia na simu kwenye chumba cha mtihani, kutumia karatasi zenye miandiko isiyolingana, na kuingia na notsi kinyume na taratibu za mitihani.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii