Wabunge wa Ufaransa wapiga kura ya kuiondoa serikali ya waziri mkuu

Wabunge wa Ufaransa Jumatano wamepiga kura ya kuiondoa serikali ya waziri mkuu Michel Barnier baada ya miezi mitatu tu ikiwepo madarakani, katika hatua ya kihistoria ambayo inaiweka tena nchi hiyo katika hali tete ya kisiasa.

Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 60, bunge la taifa limeindoa serikali iliyo madarakani, kwa kuidhinisha kura ya kutokuwa na imani na serikali iliyopendekezwa na chama cha mrengo mkali wa kushoto lakini ambayo iliungwa mkono na chama cha mrengo mkali wa kulia kinachoongozwa na Marine Le Pen.

Kuondolewa kwa haraka kwa waziri mkuu Barnier kwenye wadhifa wake kunajiri baada ya uchaguzi wa mapema wa bunge uliofanyika kipindi cha msimu wa kiangazi mwaka huu ambapo hakuna chama kilichopata wingi wa wabunge, huku chama cha mrengo mkali wa kulia kikiwa na mchango mkubwa ili serikali iweze kuendelea kuongoza.

Rais Emmanuel Macron sasa atakuwa na kibaruwa kigumu kumteua waziri mkuu mpya anayekubaliwa na pande zote wakati kukisalia miaka miwili kabla ya muhula wake kumalizika.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii