Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) limeihakikishia Serikali ya Tanzania ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa litaendelea kushirikiana nayo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi.
Hatua hiyo imetokana na namna ambavyo Serikali imekuwa ikisimamia kikamilifu matumizi ya fedha mbalimbali zinazotolewa na wadau wa maendeleo ikiwemo shirika hilo Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kusimamia ipasavyo fedha zote za maendeleo zinazoletwa nchini na kuhakikisha zinatumika kama ilivyokusudiwa.
Ameyasema hayo Mei 28, 2025 alipokutana na Makamu wa Rais wa JICA, Miyazaki Katsura kwenye ukumbi wa Mikutano wa Tachibana uliopo katika hotel ya New Otani, Tokyo nchini Japan akiwa katika ziara yake ya kikazi.
Kadhalika Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa JICA kuendelea kutafuta wadau zaidi wa maendeleo kwa ajili ya upatikanaji wa fedha zitakazowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuwafanya Watanzania kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Amesema lengo la wito huo ni kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa malengo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kuwa wanafungua milango ya kiuchumi ili wananchi wengi washiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo na kujiongezea kipato.
Waziri Mkuu amesema Serikali inataka kuona wananchi wanaendesha shughuli za kibiashara kukiwa na huduma zote katika mazingira rahisi, ikilinganishwa pia na utekelezaji wa miradi ya elimu, afya, miundombinu, nishati, ujenzi wa barabara pamoja na kilimo ni maeneo yanayotiliwa mkazo.