Bilionea na mwanzilishi mwenza wa Microsoft, Bill Gates, amemlipa aliyekuwa mke wake, Melinda Gates kiasi cha dola bilioni 8 za Kimarekani, sawa na takriban shilingi trilioni 23.12 za Kitanzania, miaka mitano baada ya ndoa yao kuvunjika kufuatia madai ya usaliti na uhusiano wake wa karibu na mfadhili aliyekuwa mtuhumiwa wa makosa ya kingono kwa watoto, Jeffrey Epstein.
Kwa mujibu wa Gazeti la The New York Times, Bill Gates alitoa dola bilioni 7.88 kwa Pivotal Philanthropies Foundation, taasisi ya misaada ya Melinda, ikiwa ni sehemu ya makubaliano makubwa ya talaka yao.
Mnamo Mei 2024, Melinda alijiuzulu rasmi kutoka Bill & Melinda Gates Foundation, taasisi waliyoianzisha na kuiendesha pamoja kwa miaka mingi.
Wakati huo, alidokeza kuwa Bill Gates angepaswa kuchangia hadi dola bilioni 12.5 kwa taasisi mpya ya misaada aliyopanga kuianzisha.
Mchango wa dola bilioni 8 kwa taasisi ya Pivotal, inayojihusisha zaidi na haki na ustawi wa wanawake, unaonekana kuwa ni awamu ya kwanza ya mchango huo mkubwa uliopendekezwa.
Bill na Melinda Gates walifunga ndoa mwaka 1994 na kuachana rasmi mwaka 2021, baada ya kupata watoto watatu.
Baada ya talaka hiyo, Melinda alimkosoa vikali Bill Gates kutokana na mahusiano yake ya kimapenzi pamoja na urafiki wake wa karibu na Jeffrey Epstein.
Kwa upande wake, Bill Gates amekiri kujutia sana uhusiano wake na Epstein, lakini amekanusha mara zote kuhusika katika vitendo vyovyote visivyo halali.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime