Udanganyifu, kuandika matusi bado tatizo katika mitihani
Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), limetangaza matokeo ya Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne na Kidato cha Pili uliofanyika Oktoba na Novemba, 2025, ambapo wanafunzi 173,015 hawajafanya upimaji huo, huku matokeo yote ya wanafunzi 89 yakifutwa kwa udanganyifu na kuandika matusi.
Kati ya matokeo yaliyofutwa, 41 ni waliofanya udanganyifu na wanane walioandika matusi kwenye scripti zao za Upimaji wa Kitaifa Darasa la Nne na kwa Kidato cha Pili waliofanya udanganyifu ni 29 na 11 walioandika matusi kwenye scripti katika upimaji huo.
Matokeo hayo yametangazwa leo Januari 10,2026, na Katibu Mtendaji wa NECTA, Prof. Said Mohamed, ambapo amesema yanahusisha wanafunzi waliopimwa kwa kuzingatia mifumo miwili ya mitaala. Amesema katika upimaji wa kitaifa wa Darasa la Nne 2025 wanafunzi wote wamefanya upimaji kwa mitaala iliyoboreshwa.
Amesema kati yao ambao hawajafanya upimaji huo, Darasa la Nne ni wanafunzi 93,309 sawa na asilimia 5.89, Kidato cha Pili ni wanafunzi 77,689 sawa na asilimia 8.74 na wanafunzi wa Kujitegemea ni 2,017 sawa na asilimia 21.33.
Prof. Mohamed amesema katika Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili 2025 wanafunzi wa mtaala wa awali walifanya upimaji kwa mtaala huo. “Wanafunzi waliokuwa wakitumia mtaala ulioboreshwa (Mkondo wa Amali) walitahiniwa kwa mara ya kwanza kwa kuzingatia mtaala ulioboreshwa,"amesema.
Prof. Mohamed amesema kwa mwaka 2026 wanafunzi wote wa Kidato cha Pili watapimwa kwa mtaala ulioboreshwa.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime
Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii