Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia Ilani yake mpya ya uchaguzi, imeahidi mageuzi makubwa ya huduma ya maji nchini katika kipindi cha miaka mitano ijayo ikiwa ni pamoja na kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi pamoja na kukuza sekta ya kilimo na ufugaji.
Akizungumza kuhusu mpango huo Mwenyekiti wa Kamati ya Ilani ya CCM Profesa Kitila Mkumbo amesema kuwa serikali itaanzisha Gridi ya Taifa ya Maji ikiwa ni hatua ya kimkakati ya kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa uwiano sawa nchi nzima kama ilivyo kwenye sekta ya umeme.
Kwa mujibu wa Prof. Mkumbo serikali inatarajia kutumia maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa pamoja na mito mikubwa ya maji, kama vyanzo vikuu vya mradi huo mkubwa wa kimkakati.
Katika hatua ya awali serikali itajenga mradi mkubwa kutoka Ziwa Victoria hadi Dodoma, utakaohusisha ujenzi wa mabomba mawili makuu—moja kwa ajili ya maji ya kunywa na lingine kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji pamoja na matumizi ya mifugo.
Kwa hatua za kukabiliana na changamoto za makazi kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita serikali itajikita zaidi katika kuboresha upatikanaji wa makazi bora kwa wananchi wa kada zote. tatizo la uhaba wa makazi bora nchini, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeweka malengo ya kuondoa kabisa nyumba za tembe ifikapo mwaka 2030.
Ikiwa ni sehemu ya mkakati wa chama hicho katika Ilani yake mpya ya uchaguzi, ambapo kinaahidi kuhakikisha wananchi wanapata nyumba za kisasa salama na zenye gharama nafuu.