Tume ya uchaguzi nchini Msumbiji inatarajiwa wakati wowote kuchapisha matokeo ya uchaguzi wa rais na bunge uliofanyika tarehe 9 mwezi huu. Hofu imetanda baada ya upinzani kuitisha maandamano kwa siku 25.
Jana Rais Filipe Nyusi alionya kwamba miito inayotolewa ya kufanyika maandamano ya kuzusha vurugu huenda ikatazamwa kama kitendo cha uhalifu. Hali ya wasiwasi imeongezeka nchini humo kabla ya matokeo ya uchaguzi kuchapishwa, ambayo yanatarajiwa kukitangazia ushindi chama tawala cha Frelimo.
Rais Nyusi amewaambia waandishi wa habari kwamba hatua za kuuchochea umma kufanya maandamano, kuupotosha ulimwengu na kutengeneza mazingira ya vurugu ni suala litakaloangaliwa kama uhalifu. Maelfu ya watu walikusanyika jana Jumatano nje ya mji mkuu Maputo katika mazishi ya wakili wa mgombea urais wa upinzani, Elvino Dias, aliyeuwawa pamoja na mshirika mwingine wa upinzani, Paulo Guambe.
Mgombea wa upinzani, Venancioa Mondlane, ambaye amedai wakili wake aliuwawa kwa kupigwa risasi mara 25 na vikosi vya usalama, amesema ataanzisha siku 25 za harakati nchini humo kupinga mauaji hayo.