Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump amesema hatashiriki mdahalo mwingine na mpinzani wake Kamala Harris. Ingawa kura za maoni zilionyesha kuwa Harris alishinda mdahalo wa kwanza, Trump aliona mambo kwa njia tofauti.
Trump alitoa msimamo huo baada ya yeye Harris kurejea kwenye kampeni zao katika majimbo yenye maamuzi ambako yumkini kinyang'anyiro kikali cha kuingia ikulu ya White House kitaamuliwa mwezi Novemba.
Rais huyo wa zamani wa chama cha Republican alichapisha ujumbe kwenye mtandao wake akidai kuwa alishinda mdahalo wa Jumanne, ingawa uchunguzi wa maoni ulionyesha Harris alishinda mdahalo huo.
"HAKUTAKUWA NA MDAHALO WA TATU!" Trump mwenye umri wa miaka 78 aliandika kwenye jukwaa lake la Truth Social, akijumlisha pia mjadala wa awali na Joe Biden mwezi Juni ambao uliiweka pabaya sana nafasi ya rais huyo alieko madarakani kuchaguliwa tena.
"Kura za maoni zinaonyesha wazi kwamba nilishinda Mjadala dhidi ya Komredi Kamala Harris," Trump alisema, licha ya kura kadhaa kuonyesha Harris akiibuka mshindi katika mdahalo huo ulioandaliwa na ABC, na kutazamwa na watazamaji wapatao milioni 67.
Wademokrat walikuwa wamemtaka Trump akubali kushiriki mdahalo wa marudio baadaye.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni katika jimbo la North Carolina, mgombea wa Democratic Harris, alisisitiza kuwa wawili hao wanapaswa kujadiliana tena kabla ya uchaguzi wa Novemba 5.