Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amewasili jijini Jeddah, Saudi Arabia na kupokelewa kwa heshima zote na Mrithi wa Kiti cha Ufalme, Mwanamfalme Mohammed bin Salman, katika jumba la kifalme, jana, Jumatatu, Machi 10, 2025.
Zelensky na ujumbe wake kutoka Ukraine wanatarajiwa kukutana na mwanadiplomasia wa juu wa Marekani nchini Saudi Arabia kujadili namna ya kumaliza vita vya miaka mitatu na Urusi.
Katika mazungumzo hayo, Ukraine inapanga kupendekeza usitishaji wa mapigano katika Bahari Nyeusi, kusitisha mashambulizi ya makombora ya masafa marefu, pamoja na kuachiliwa kwa wafungwa wa vita, maafisa wawili waandamizi wa Ukraine walisema.
Maafisa hao, ambao walizungumza kwa sharti la kutotajwa majina kwa sababu hawakuwa na ruhusa ya kuzungumzia kikao hicho hadharani, waliiambia Shirika la Habari la Associated Press kuwa ujumbe wa Ukraine uko tayari kusaini makubaliano na Marekani kuhusu upatikanaji wa madini adimu ya Ukraine.
Makubaliano hayo ni jambo ambalo Rais wa Marekani, Donald Trump, anataka kuhakikisha yanafikiwa.
Mazungumzo hayo yanahusu hatua za kujenga imani kati ya pande husika, ingawa maafisa hao hawakutoa maelezo zaidi.
Timu ya mazungumzo ya Ukraine inatarajiwa kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, katika mji wa Jeddah.
Kyiv inajaribu kurekebisha athari zilizotokana na ziara ya Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, jijini Washington mnamo Februari 28, ambapo mazungumzo yake katika Ikulu ya Marekani yaligeuka kuwa mvutano kati yake, Trump, na Makamu wa Rais JD Vance.
Kinachozingatiwa katika mazungumzo haya ni msaada wa kijeshi na kijasusi ambao Marekani ilikuwa imetoa kwa Ukraine katika vita hivyo, lakini sasa umesitishwa huku Washington ikishinikiza makubaliano ya amani.
Rubio na Zelensky waliwasili Saudi Arabia kwa nyakati tofauti jana, Jumatatu, lakini hawakukutana.
Hata hivyo, Zelensky alikutana na mwanamfalme mwenye ushawishi wa Saudi Arabia jioni ya Jumatatu.
Rais huyo alisema kuwa walifanya mazungumzo ya kina kuhusu hatua na masharti muhimu ya kumaliza vita hivyo na kuhakikisha amani ya kudumu.