Rais wa zamani wa Ufilipino, Rodrigo Duterte amekamatwa kwa hati maalum kutoka Mahakama ya Uhalifu wa Kivita (ICC) kufuatia tuhuma za ukatili dhidi ya binadamu zinazomkabili.
Duterte amekamatwa leo Jumanne katika Uwanja wa Ndege wa Manila muda mfupi baada ya kuwasili akitokea Hong Kong.
Serikali ya Ufilipino imeeleza kuwa ilipokea hati ya kukamatwa kwa Duterte kutoka Mahakama ya ICC na Interpol na kwamba kwa sasa anashikiliwa akisubiri kukabidhiwa kwa ICC.
Miongoni mwa mashtaka yanayomkabili, ni pamoja ukatili mkubwa anaodaiwa kuuendesha katika oparesheni kali ya kupambana na dawa za kulevya aliyoiendesha kuanzia mwaka 2016 hadi 2022 alipokuwa madarakani ambapo inaelezwa kuwa watuhumiwa wengi wa biashara hiyo, waliuawa kikatili.