Tanzania Yajibu Azimio la Bunge la Ulaya Kuhusu Kesi za Kisheria, Yasisitiza Uhuru wa Mahakama

Serikali ya Tanzania imetoa tamko kuhusu azimio lililopitishwa na Bunge la Ulaya tarehe 8 Mei 2025 kuhusu kesi za kisheria zinazoendelea nchini, ikieleza kutoridhishwa na hatua hiyo kwa kuwa Bunge hilo limetoa maamuzi kwa kuzingatia taarifa za upande mmoja bila kushauriana kwa njia za kidiplomasia na Tanzania.

Serikali imeeleza kuwa haiwezi kuingilia mhimili wa Mahakama.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inasema, “Ingawa Tanzania inaheshimu uhuru wa kitaasisi wa Bunge la Ulaya na inathamini ushirikiano wake na Umoja wa Ulaya, bado inaona kuna umuhimu wa kufafanua baadhi ya mambo na kusisitiza msimamo wake wa muda mrefu kuhusu maadili ya kidemokrasia, utawala bora, na utawala wa sheria.”

Wizara hiyo imeeleza kuwa tangu Machi 2021, Tanzania imefanya mageuzi makubwa ya kisiasa na kisheria chini ya falsafa ya 4Rs, ambayo yamezaa matokeo chanya ikiwa ni pamoja na kurejesha uhuru wa kisiasa, kupanua haki za raia, kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari, na kupitishwa kwa sheria mpya za uchaguzi Machi 2024 ambazo zimepelekea kuanzishwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Aidha, taarifa hiyo imesisitiza kuwa Tanzania ni nchi huru inayoongozwa na katiba yake, ambapo masuala ya kisheria yanashughulikiwa kwa uhuru na mhimili wa Mahakama kwa mujibu wa sheria za kitaifa na viwango vya kimataifa. Serikali imeeleza kuwa, “Mhimili wa Serikali hauwezi kuingilia kesi zinazoendelea Mahakamani, na hivyo kauli zinazohimiza Serikali iingilie utendaji wa Mahakama sio tu hazifai bali pia zinakinzana na misingi ya katiba kuhusu uhuru wa Mahakama.”

Serikali ya Tanzania pia imeonesha wasiwasi kuhusu mwelekeo unaoonekana wa baadhi ya wadau wa kimataifa kutoa maoni kuhusu kesi za kisheria nchini bila kufanya mashauriano ya kidiplomasia. Aidha, taarifa hiyo imebainisha kuwa maendeleo yaliyopatikana katika maeneo kama uhuru wa vyombo vya habari, ushirikishwaji wa kisiasa, mageuzi ya uchaguzi, na ujenzi wa amani wa kikanda hayakuzingatiwa kwenye maoni ya Bunge la Ulaya.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii