Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika amesema Chama hicho hakijaridhishwa na maamuzi yaliyotolewa na Mahakama katika shauri linaloendelea baada ya Mahakama kutakataa maombi ya Chama hicho ya kutengua amri yake ya Chama kuzuiliwa kufanya shughuli za kisiasa, akisema kuwa bado kuna mambo ya msingi ya haki ambayo hayajatendeka.
Akizungumza na Waandishi wa Habari August 18 baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es salaam kutupilia mbali maombi hayo ya CHADEMA, amesema kwa ushauri wa kisheria walioupata, maamuzi hayo yanaangukia katika kundi la maamuzi yanayojulikana kama Interlocutory orders, ambayo kisheria hayawezi kukatiwa rufaa wakati kesi ya msingi bado haijasikilizwa.
“Hatuwezi kukata rufaa sasa kwa sababu haya ni maamuzi ya awali, lakini iwapo lolote litakalotokea kwenye kesi ya msingi litasababisha haki kukosekana, tutachukua hatua stahiki,” alisema Mnyika.
Aidha, alibainisha kuwa kesi ya msingi inatarajiwa kuanza kusikilizwa kuanzia tarehe 28 Agosti, na baada ya hapo ndipo Chama kitaamua rasmi kupeleka shauri hilo Mahakama ya Rufaa.
Uamuzi huo umetolewa leo na Jaji Hamidu Mwanga baada ya kupitia hoja za walalamikaji na walalamikiwa juu ya maombi yao na miongoni mwa maombi ya CHADEMA ambayo waliiomba Mahakama itengue amri zake mbali ya kuzuiwa kufanya shughuli za kisiasa, pia waliomba iruhusu kutumia rasilimali za Chama hicho.