Wasomi wa Kiswahili wamuomboleza Profesa Hamu Habwe
WAPENZI wa Kiswahili nchini na kanda nzima ya Afrika Mashariki wanaomboleza kifo cha msomi na mwandishi Profesa John Hamu Habwe ambaye alifariki akiwa na umri wa miaka 62.
Profesa Habwe alifariki akitibiwa Jumapili, Agosti 17, 2025 katika hospitali moja jijini Nairobi baada ya kuugua kwa zaidi ya miaka mitatu.
Profesa Habwe ambaye alizaliwa katika Kijiji cha Ebukhaya, Emabuye kaunti ndogo ya Emuhaya ni Profesa wa kwanza katika kata ya Ebukhaya.
Kwa mujibu wa kakake mdogo Astaricus Hamu ni kwamba marehemu alikuwa nguzo muhimu katika familia yao.
“Profesa alikuwa nguzo muhimu katika jamii yetu hatujawahi kuwa na mtu msomi mwenye kujali watu wake kama ndugu yangu. Mungu ailaze roho yake pema peponi.” alisema.
Profesa Habwe alianzia masomo yake katika Shule ya Msingi ya Ebukhaya katika iliyokuwa kata ya North Bunyore miaka ya sabini kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Ebwali East Bunyore miaka ya themanini na hatimaye kujiunga na shule ya upili ya Kapkatet Boys kaunti ya Kericho kwa Kidato cha Sita.Alijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi idara ya Lugha ya Kiswahili mapema miaka ya tisini kabla ya kufundisha katika shule mbalimbali eneo la Bunyore na hatimaye kuwa mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Nairobi.
Amefundisha katika chuo hicho kwa zaidi ya miaka 30 hadi mwaka wa 2016.
Alipokuwa UoN alipata kuhudumu kama Mwenyekiti wa Idara ya Kiswahili na lugha zingine za Kiafrika kwa miaka miwili.
Mbali na kuwa mwalimu, ameandika vitabu kadha na kushiriki warsha za Kiswahili na kutoa ushauri kwa wataalamu wa lugha ya Kiswahili kupitia kwa vipindi vya redio na runinga haswa KBC.
Marehemu aliwahi kufundisha katika vyuo vingine ikiwa ni Pamoja vyuo vikuu vya Moi, Maseno na chuo kikuu cha Catholic.
Vile vile, alifanya kazi katika mashirika ya kimataifa kama vile Shirika la Chakula na Kilimo FAO, Shirika la Afya Duniani, WHO na Tume ya Kiswahili Afrika Mashariki yani Kiswahili Commission of East Africa kama mtafsiri.
Aliandika vitabu vya watoto miongoni mwa vitabu vingine ikiwa ni pamoja na kitabu chake cha kwanza ‘Maumbile si huja’.
Mipango ya mazishi inaendelea; atazikwa katika shamba lake Lugari katika Kaunti ya Kakamega.
Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii