RAIS wa Syria, Ahmed al-Sharaa, amesema juhudi za kuunganisha taifa hilo baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe hazipaswi kufanyika kwa njia ya umwagaji damu.
Akihutubia kupitia televisheni ya taifa, kiongozi huyo alipinga mgawanyiko wowote wa nchi na kuishutumu Israel kwa kuingilia masuala ya Syria upande wa kusini.
Kauli hiyo imetolewa wakati maandamano yakiendelea mkoani Sweida, kusini mwa nchi hiyo, ambapo mamia ya raia waliandamana wakilaani ghasia za kimadhehebu zilizotokea mwezi uliopita na kudai haki ya kujitawala kwa mkoa huo unaokaliwa na watu wa madhehebu ya Druze.
Waandamanaji wengine walionekana wakipeperusha bendera ya Israel, wakitaka kujitenga. Mapema, mapigano makali kati ya Wadruze na Wabedui wa Kisunni yalichochea hali ya taharuki, huku vikosi vya serikali na mashambulizi ya Israel yakiongeza ukali wa mzozo huo.