WAUMINI WA DINI YA KISLAAM WAASWA KUPELEKA WATOTO SHULE

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amir Mkalipa, amewaasa waumini wa dini ya Kiislamu pamoja na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanawapeleka watoto shule ili wapate elimu ya dini na dunia.


Akizungumza katika viwanja vya Nyamagana, kwenye kongamano la Hija lililoandaliwa na Taasisi ya Biitha, Mkalipa amesema ili taifa liwe na jamii bora ya wasomi, ni lazima wazazi wahakikishe watoto wao wanasoma ili wawe msaada mkubwa kwa nchi.


Aidha, amewataka masheikh na maimamu kuanzisha utaratibu wa kutoa elimu ya umuhimu wa hija katika misikiti na madrasa, ili kuongeza idadi ya mahujaji wanaokwenda Makka kutekeleza nguzo ya tano ya Uislamu.

Kongamano hilo limezinduliwa rasmi katika uwanja wa Nyamagana, jijini Mwanza, Jumamosi ya tarehe 16 Agosti mwaka huu, na litaendelea kufanyika katika mikoa mbalimbali ya Kanda ya Ziwa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii