MKAZI wa Kijiji cha Magugu, John Claude (24), maarufu 'mdogoo" amefikishwa Mahakama ya Wilaya ya Babati, mkoani Manyara, akikabiliwa na mashtaka ya kumbaka na kumwingilia kinyume cha maumbile, mwanafunzi wa kidato cha pili.
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mwishoni mwa wiki na Mwendesha Mashtaka wa Serikali Mwanaidi Chuma, inadaiwa kuwa mshtakiwa Claude anakabiliwa na makosa mawili ya kubaka kwa kundi na kulawiti.
Kwa mujibu wa hati hiyo ya mashtaka, kosa la kwanza la kubaka kwa kundi, ni kinyume cha Kifungu cha 130 (1),(2)e na (1) kikisomwa na Kifungu cha 131A(1)(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Wakati, kosa la pili la kulawiti ni kinyume cha Kifungu cha 154 (1)(a) na (2) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Ilidaiwa mahakamani huko na Wakili Chuma, kwamba mshtakiwa Juni 7 mwaka huu, akiwa Kijiji cha Magugu, alifanya mapenzi na mtoto huyo (jina limehifadhiwa) kwa kumwingilia kinyume na maumbile.
Aidha, iliendelea kudaiwa mahakamani huko kwamba, siku ya tukio kulitokea ugomvi baina ya mama wa mtoto huyo na baada ya ugomvi, ndipo mtoto aliondoka na kwenda kwa shangazi yake na akiwa njiani alikutana na watu wawili wakiwa kwenye pikipiki walitaka kumpa lifti ila alikataa.
Mshtakiwa alimchukua kwa nguvu na kumpandisha katika pikipiki na kumpeleka Kijiji cha Magugu na baadaye yeye na wenzake walimbaka na kumlawiti mtoto huyo.
Mshtakiwa aliposomewa mashtaka hayo, alikana mashtaka yote. Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Babati, Mossy Sasi, aliahirisha shauri hilo hadi Agosti 21 mwaka huu itakapotajwa tena mahakamani hapo.