MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),imesema kuwa kupitia mifumo ya ukaguzi na ufuatiliaji wa bidhaa katika soko iliyowekwa imebaini uwepo katika soko wa Dettol za maji bandia zenye ujazo wa 50ml, 125ml, 250ml, 500ml na Lita1 zinazotengenezwa kinyume cha Sheria (njia haramu) na kubandikwa lebo kuonesha kwamba ni Dettol zilizo halisi.
Taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Mkurugenzi Mkuu TMDA,Dkt. Adam Fimbo imesema kuwa utengenezaji wa Dettol hizo bandia umebainika kufuatia taarifa za kiintelijensia zilizokusanywa na TMDA na kisha ukaguzi uliofanywa kwa pamoja na Jeshi la Polisi katika nyumba moja ya kulala wageni inayoitwa New Kishimbe Lodge iliyopo Mtaa wa Namanga, Kahama mjini, mkoa wa Shinyanga.
Imesema taarifa hiyo kuwa katika nyumba hiyo kulikutwa malighafi mbalimbali zikiwemo vifaa, kemikali na vyombo kama vile chupa tupu za Dettol, lebo, rangi, madumu makubwa na vimiminika (liquid foams) katika chumba kimojawapo walichokuwa wanaishi raia wawili kutoka nchi jirani ambao wanatuhumiwa kushiriki katika uhalifu huo.
“Ili uweze kutambua Dettol ni bandia utabaini baadhi ya Dettol bandia zimegushiwa namba za matoleo (batch numbers) na kuandikwaP08 08 24R25 na P08 02 24R25 ,kifuniko hakina kifungo (lock) kinachounganisha na bangili ya chini. Hivyo kinafunguka kirahisi, Lebo zinafanana na halisi lakini za Dettol bandia zinabanduka kirahisi sana,”ilisema sehemu ya taarifa hiyo
Imesema TMDA inawashauri wananchi wote wanaotumia Dettol za maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya kuuwa vijidudu kuangalia kwa makini lebo zake na endapo watatilia mashaka watoe taarifa kwenye Ofisi za TMDA zilizo karibu au Kituo cha Polisi.
Aidha, wafanyabiashara wanaojihusisha na ununuzi wa bidhaa hizi, wanaelekezwa kununua Dettol kutoka katika vyanzo halisi na kupewa risiti kwa manunuzi waliyofanya.
“Watuhumiwa waliohusika na uhalifu huu wamefikishwa katika vyombo vya usalama na tararibu za kuwafikisha Mahakamani zinaendelea ili kuweza kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.
“TMDA inatoa onyo kwa kampuni, kikundi, mitandao au mtu yeyote anayejihusisha na utengenezaji, usambazaji au uuzaji wa dawa ikiwemo vipukusi (antiseptics and disinfectants), vifaa tiba na vitendanishi duni na bandia kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,”imesema
Aidha, imesema TMDA inaendelea kutoa wito kwa wananchi wote kuendelea kutoa taarifa TMDA au Vituo vya Polisi wanapobaini uwepo wa ukiukwaji ya Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba Sura 219 ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa lengo la kulinda afya ya jamii.