Trump achelewesha ushuru wa Mexico baada ya kuzungumza na Rais Sheinbaum

Rais wa Marekani Donald Trump Alhamisi amechelewesha kwa wiki nne ushuru mpya wa asilimia 25 kwenye bidhaa nyingi kutoka Mexico na Canada kwa mauzo yake kuja  Marekani.

Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wake wa karibu katika vita vya biashara vya Amerika Kaskazini ambavyo vimelifanya soko la hisa kuanguka kwa siku kadhaa na kusababisha mivutano ya uhusiano wa Marekani na washirika wake wa muda mrefu na pia washirika wawili wakubwa sana wa kibiashara.

Trump kwanza alichelewesha ushuru wa bidhaa kutoka Mexico kuja Marekani hadi Aprili 2 baada ya kumsikia moja kwa moja Rais wa Mexico, Claudia Sheinbaum, akisema jinsi serikali yake imesaidia kuzuia mtiririko wa wahamiaji na dawa haramu za fentanyl kuingia Marekani, madai mawili yaliyotolewa na Marekani kwa Jirani yake wa kusini.

Saa kadhaa baadaye, pia alisitisha ushuru mpya kwa Canada, ingawaje kitakachotokea kwa ushuru baada ya mwezi mmoja hakijulikani. Hatua za Trump za karibuni zimekuja siku moja baada ya kusimamisha ushuru kwa muda kwa magari yanayoagizwa kutoka katika nchi hizo mbili baada ya watengenezaji magari watatu wakubwa nchini Marekani kusema ushuru huenda ukawa na athari mbaya za kifedha kwa kampuni zao.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii