Asilimia 90 Ya Kipato Cha Mwanamke Hutumika kwa Ajili Ya Familia

Katika kusherehekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), David Kafulila, kama ilivyo kawaida yake kupenda takwimu na tafiti, ameungana na wanawake kwa kutoa ripoti tatu za tafiti.

Akianza na ripoti ya taasisi ya UNAC, amesema inaonesha kuwa asilimia 90 ya kipato cha mwanamke kinatumika kwa matumizi ya familia, ikilinganishwa na asilimia 35 ya kipato cha mwanaume huko Marekani.

Kafulila anahoji kama hali hiyo ni sawa kwa Tanzania?

Akiendelea kutoa sifa kwa wanawake, Kafulila ametumia Ripoti ya McKinsey inayoeleza kuwa laiti kungekuwa na usawa katika nafasi za uongozi duniani, tija yake ingeongeza dola trilioni 28 kwenye uchumi wa dunia.

Kafulila amehitimisha salamu zake kwa Siku ya Wanawake kwa kutumia ripoti ya Women Count Report 2020, inayoonesha kwamba katika kampuni kubwa 350 kwenye soko la mitaji la London, ni kampuni 14 pekee zinazoongozwa na wanawake.

Hata hivyo, kampuni ambazo walau theluthi moja ya viongozi wake wa ngazi ya juu ni wanawake zinapata faida mara 10 zaidi ikilinganishwa na kampuni ambazo wanawake wamepewa umuhimu mdogo kwenye nafasi za uongozi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii