Mahakama ya Wilaya Bariadi mkoani Simiyu imemhukumu kifungo cha miaka 20 jela pamoja na kuchapwa viboko 12 Emmanuel John (31), maarufu kama Chief wa Kilulu, kwa kosa la kukutwa na nyara za serikali aina ya fisi akiwa hai na akiishi naye nyumbani kwake.
Mshtakiwa huyo, ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kilulu kilichopo kata ya Bunhamala, wilayani Bariadi, na mganga wa kienyeji, alipewa adhabu hiyo katika kesi namba 2458/2025 iliyokuwa ikimkabili kwenye mahakama hiyo.
Hukumu hiyo imetolewa jana na hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo, Caroline Kiliwa, mara baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.
Awali, akisoma kosa la mshtakiwa, Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mashtaka Mkoa, Lupiana Mahenge, alieleza mahakama kuwa mtuhumiwa huyo alikutwa na nyara ya serikali, fisi akiwa hai, akimfuga nyumbani kwake kinyume cha sheria.
Alisema kuwa mnamo Januari 1, 2025, katika eneo la kijiji cha Kilulu, mtuhumiwa alikamatwa kufuatia Jeshi la Polisi kupata taarifa kutoka kwa raia wema, ambao waliripoti kuhusu mtuhumiwa kuishi na fisi hai ndani ya nyumba yake.
Alieleza kuwa mtuhumiwa aliishi na fisi huyo kama mnyama wa kufuga kinyume na kifungu cha 86 (1) na kifungu kidogo cha (2)(C)(III) cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori sura ya 283, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Alisema kuwa kifungu hicho kinasomeka pamoja na kifungu cha 14, jedwali la kwanza na kifungu cha 57 (1), na kifungu cha 60 (2) cha Sheria ya Kupambana na Uhujumu Uchumi sura ya 200, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Upande wa mashtaka, katika kuthibitisha kosa hilo, ulipeleka mashahidi sita ambao waliithibitishia mahakama pasipo kuacha shaka.
Mtuhumiwa alipopewa nafasi ya kujitetea aliomba mahakama imsamehe kwa kuwa anategemewa na familia ya watoto wanne, wakiwemo mapacha, ndipo hakimu akatoa adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela na viboko 12 ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine.