Guardiola afunguka mafanikio 2023/24

Kocha wa Mabingwa wa Soka nchini England Manchester City Pep Guardiola ametajwa kuwa Kocha Bora wa Msimu wa 2023/24 kwenye Ligi Kuu ya England.

Guardiola aliiongoza Manchester City kutwaa taji la nne mfululizo la Ligi Kuu ta England mwishoni mwa juma lililopita, kwa kuifunga West Ham Utd mabao 3-1, Uwanja wa Etihad mjini Manchester.

Kocha huyo kutoka nchini Hispania alitajwa kuwa mshindi wa Tuzo hiyo usiku wa kuamkia leo, ambapo baadaye alisema: “Ni heshima kutajwa kuwa Kocha Bora wa Ligi Kuu ya England.

“Tuzo hii inaonyesha bidii na ubora wa watu katika Klabu na idara zote. Ninajivunia kuwa meneja wa Kundi la Wachezaji wangu na kufanya kazi pamoja na Makocha mahiri na Wafanyikazi wa klabu.

“Kushinda mataji manne mfululizo ni mojawapo ya mafanikio ya kujivunia katika taaluma yangu. Hii ni ligi ngumu zaidi duniani na washindani wetu wamecheza soka la ajabu.

“Nilipowasili England, sikuwahi kufikiria kuwa pamoja tunaweza kushinda Ligi Kuu mara sita ndani ya miaka saba.

“Tumefanya kitu kisichoaminika na kusherehekea na mashabiki wetu, Jumapili iliyopita ilikuwa siku ambayo nitaikumbuka daima.”

Naye Mkurugenzi wa Soka wa Man City Txiki Begiristain aliongeza: “Kila mtu katika Klabu hii anafurahishwa na Pep na utambuzi huu wa hivi punde wa mafanikio yake.

“Kama Pep huwa mwepesi kusema, historia yetu ya kufaulu ni juhudi ya timu na isingewezekana bila bidii ya wachezaji wetu, makocha na wafanyikazi wetu.

“Hata hivyo, uongozi wa Pep wenye msukumo wa kufanikiwa umetufanya kuwa timu nzuri ya kutazama na kutuona kwa mara nyingine tena tukitoka kileleni kwenye ligi hiyo ngumu zaidi duniani.

“Ameipeleka Klabu kwenye kilele cha mchezo na kila mtu aliyeunganishwa na Manchester City anapaswa kujivunia kwamba anatuwakilisha.”

Kocha wa Arsenal Mikel Arteta, Unai Emery wa Aston Villa, Andoni Iraola wa Bournemouth na Jurgen Klopp wa Liverpool walikuwa washindani wa Pep Guardiola kwenye tuzo hiyo msimu huu 2023/24.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii