Real Madrid imepokea pigo baada ya kiungo wake nyota, Jude Bellingham, kupata jeraha la misuli litakalomuweka nje ya uwanja kwa muda.
Nyota huyo wa England alipata maumivu ya ghafla katika misuli ya nyuma ya paja (hamstring) mapema tu katika mchezo dhidi ya Rayo Vallecano, baada ya kufanya mbio kuelekea mstari wa mwisho wa uwanja. Mara moja alionekana kushika mguu wake wa kushoto na kulazimika kutolewa nje huku akionyesha maumivu makali.
Uchunguzi wa kitabibu uliofanywa na madaktari wa Real Madrid umethibitisha kuwa Bellingham ameumia misuli ya semitendinosus kwenye mguu wake wa kushoto.
Awali, klabu hiyo ilikadiria kuwa kiungo huyo atakaa nje kwa takribani mwezi mmoja. Hata hivyo, mwandishi wa habari Ramón Álvarez de Mon ameonya kuwa muda wa kupona unaweza kuongezeka hadi miezi miwili — hali ambayo itakuwa pigo kubwa kwa kikosi cha Carlo Ancelotti.
Iwapo atakosekana kwa muda mrefu, Bellingham ataikosa Real Madrid katika mechi muhimu za LaLiga dhidi ya Real Sociedad, Osasuna, Getafe, Celta Vigo, Elche na Atlético Madrid. Pia hatakuwepo kwenye mchujo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Benfica pamoja na hatua ya 16 bora iwapo Los Blancos watafuzu.
Hata hivyo Jeraha hilo linaongeza presha kwa benchi la ufundi la Real Madrid wakati kikosi hicho kikijiandaa na ratiba ngumu ya mashindano ya ndani na Ulaya.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime