EU Yataka Uchunguzi wa Ukiukwaji wa Haki Uganda

Bunge la Umoja wa Ulaya limetaka kufanyika kwa uchunguzi huru na wa haraka dhidi ya kile limekitaja kuwa ni uhalifu wa kibinadamu unaotekelezwa na vyombo vya usalama pamoja na baadhi ya viongozi wa kisiasa nchini Uganda.

Katika kikao chake cha Alhamisi, bunge hilo limeeleza wasiwasi wake kuhusu ushindi wa Rais Yoweri Museveni, likisema kuwa uchaguzi wa mwezi uliopita uligubikwa na ukiukwaji wa haki za binadamu, vitisho kwa wapiga kura, madai ya wizi wa kura, vurugu pamoja na kufungwa kwa mitandao ya kijamii.

Aidha, wabunge wa Umoja wa Ulaya wametaka viongozi wa upinzani wanaoendelea kuzuiliwa kuachiwa huru mara moja, pamoja na kusitishwa kwa vitisho dhidi ya kiongozi wa upinzani Bobi Wine. Pia wamekemea matumizi ya nguvu na vurugu yaliyoripotiwa wakati wa mchakato wa uchaguzi.

Katika upigaji kura wa azimio hilo, wabunge 514 waliunga mkono hoja hiyo huku 56 wakikosa kushiriki.

Kauli ya Bunge la Ulaya inakuja wakati Bobi Wine akiripotiwa kuwa mafichoni kufuatia uchaguzi huo, akieleza hofu ya kukamatwa na vyombo vya usalama.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii