Watu wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Musoma mkoani Mara wakikabiliwa na mashtaka ya kuhusika na wizi wa gari la kubeba wagonjwa la Manispaa ya Musoma na kulibadilisha matumizi kuwa gari la biashara ya kubeba watalii.
Washtakiwa hao wamefikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Hadija Masala, leo Ijumaa Februari 13 mwaka huu na kusomewa mashtaka matatu, likiwemo kosa la uhujumu uchumi.
Akisoma mashtaka mahakamani hapo, Wakili wa Serikali Michael Kayombo amesema washtakiwa wote wanakabiliwa na kosa la utakatishaji wa fedha kinyume cha kifungu cha 12(d) na 13(a) cha Sheria ya Udhibiti wa Utakatishaji wa Fedha, Sura ya 423, kinachosomwa pamoja na kifungu cha 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi na Udhibiti wa Uhalifu wa Kupanga.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa pamoja, wakilitumia gari hilo la Serikali kwa manufaa binafsi baada ya kulibadilisha matumizi yake kinyume cha sheria.
Hata hivyo kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe itakayopangwa na mahakama kwa ajili ya hatua nyingine za kisheria.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime