Manchester United wanaonekana kuendelea na mipango yao ya muda mrefu bila kumjumuisha Marcus Rashford, huku hatma ya mshambuliaji huyo ikizidi kuelekea kwenye uuzaji wa kudumu badala ya kurejea Old Trafford.
Rashford kwa sasa anaitumikia Barcelona kwa mkopo wa msimu mzima, ambapo klabu hiyo ya La Liga ina kipengele cha kumnunua moja kwa moja kwa pauni milioni 26 endapo itaridhishwa na kiwango chake.
Licha ya dirisha la usajili la majira ya baridi kufunguliwa, United hawakuwa na mpango wowote wa kumrudisha nyota huyo kikosini. Kocha mkuu wa muda, Michael Carrick, ambaye aliwahi kufanya kazi na Rashford kwa zaidi ya miaka mitatu katika benchi la ufundi, ameripotiwa kutoonyesha nia yoyote ya kumrejesha.
Vyanzo vya karibu na klabu vinaeleza kuwa Carrick kwa sasa anaangazia zaidi kumaliza msimu huu, hasa ikizingatiwa mkataba wake unaisha mwishoni mwa msimu, hivyo hafanyi maamuzi ya muda mrefu kuhusu mustakabali wa wachezaji.
Wakati huohuo, viongozi wa klabu akiwemo Mtendaji Mkuu Omar Berrada na Mkurugenzi wa Soka Jason Wilcox, wanaendelea na mchakato wa kutafuta kocha wa kudumu, lakini msimamo kuhusu Rashford umebaki palepale.
Rashford hajacheza tena mechi ya United tangu Desemba 2024, na katika kipindi hicho alipoteza pia jezi namba 10 iliyochukuliwa na Matheus Cunha chini ya kocha wa zamani Ruben Amorim. Kabla ya kuondoka, Amorim aliwahi kumtenga pamoja na baadhi ya wachezaji kwa kuwaweka kwenye ratiba tofauti ya mazoezi ya kikosi cha kwanza.
Kutokana na kuondoka kwake pamoja na kuuzwa kwa Alejandro Garnacho, United sasa wanakabiliwa na upungufu wa mawinga wa asili, hali inayowalazimu kuingia sokoni kutafuta mshambuliaji mpya wa pembeni majira ya joto.
Kwa upande mwingine, Jadon Sancho yupo kwenye mkopo wake wa tatu akiwa Aston Villa na anatarajiwa kuondoka rasmi mkataba wake utakapomalizika mwezi Juni.
Hata hivyo itakumbukwa kuwa Rashford mwenye umri wa miaka 28 bado ana mkataba United hadi 2028, lakini dalili zote zinaonyesha kuwa uuzaji wa kudumu ndio njia inayotarajiwa zaidi msimu ujao, huku kurejea Old Trafford kukionekana kuwa na nafasi ndogo.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime