Lukashenko alitoa matamshi hayo baada ya kupiga kura katika uchaguzi wa bunge na madiwani, uliokosolewa na Marekani kuwa upuuzi.
Afisa mkuu anayesimamia uchaguzi katika taifa hilo la zamani la Kisovieti alitupilia mbali ukosoaji huo na kuiambia Washington ishughulikie masuala yake ya ndani.
Shirika la habari la BelTA lilisema Lukashenko, ambaye yuko madarakani tangu mwaka wa 1994, aliwaambia waandishi wa habari “ Waambie wapinzani walioko uhamishoni kwamba ntawania tena. Hakuna yeyote, rais anayewajibika ambaye anaweza kutowajali wananchi wake waliomuunga mkono katika vita hivi.”
Lukashenko, mwenye umri wa miaka 69, ni mmoja wa washirika wa karibu sana wa Rais wa Russia Vladimir Putin na ambaye aliiruhusu Kremlin kutumia aridhi ya nchi yake kuanzisha uvamizi dhidi ya Ukraine mwaka wa 2022.
“Bado tuna mwaka mmoja kabla ya uchaguzi wa rais. Mambo mengi yanaweza kubadilika,” alisema akijibu suali lingine, BelTA iliripoti.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani ililaani kile ilichotaja kuwa “uchaguzi wa kipuuzi” nchini Belarus jana Jumapili.